Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia
salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw. John Mongella kufuatia
vifo vya watu 13 vilivyosababishwa na ajali ya barabarani iliyotokana na
basi la abiria la Kampuni ya Super Shem kuligonga basi dogo la abiria
(Daladala) katika kijiji cha Mwamaya kilichopo katika Kata ya
Hungumalwa, Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza.
Ajali
hiyo imetokea tarehe 21 Septemba, 2016 Majira ya saa 12:15 Asubuhi
baada ya basi hilo dogo lililokuwa likitoka Kijiji cha Shirima kwenda
Nyegezi Mjini Mwanza kuingia ghafla barabara kuu na kisha kugongwa na
basi la Kampuni ya Super Shem lililokuwa likitoka Mkoani Mbeya kwenda
Mwanza.
Katika ajali hiyo watu wote 13 waliopoteza maisha na majeruhi 15 waliolazwa hospitali walikuwa abiria wa basi dogo lililogongwa.
Rais
Magufuli ameelezea kupokea taarifa za ajali hiyo kwa mshituko mkubwa
hasa ikizingatiwa kuwa imetokea ikiwa ni siku moja tu tangu Watanzania
wengine 12 wapoteze maisha katika ajali ya basi la Kampuni ya New Force
iliyotokea katika kijiji cha Lilombwi, Kata ya Kifanya, Tarafa ya
Igominyi Mkoani Njombe.
“Nimesikitishwa
sana na vifo vingine vya watanzania wenzetu waliopoteza maisha katika
ajali huko Mwanza, nakuomba Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw. John Mongella
unifikishie salamu za pole kwa familia zote zilizopoteza ndugu, jamaa na
marafiki katika ajali hii.
“Nawaombea
wote waliotangulia mbele za haki wapumzishwe mahali pema na pia wote
walioguswa na msiba wawe na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu
katika kipindi kigumu cha majonzi ya kuondokewa na jamaa zao” Amesisitiza Rais Magufuli.
Rais
Magufuli pia amewaombea majeruhi wote wa ajali hii wapone haraka ili
waungane na familia zao na kuendelea na shughuli za ujenzi wa Taifa.
Sign up here with your email
ConversionConversion EmoticonEmoticon