Kwa
mara ya kwanza mawaziri 11 wamekutana kwa ajili ya kutokomeza vitendo
vya ukatili wa kijinsia, huku Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto ikiweka wazi mpango wake wa kuanzisha madawati
ya kuwalinda watoto katika shule za msingi na sekondari.
Aidha, ina mpango wa kuanzisha kamati za ulinzi na usalama wa mtoto katika kila mtaa na kijiji nchi nzima, lengo likiwa ni kutokomeza vitendo vya ukatili na unyanyasaji kwa watoto.
Mawaziri
hao walikutana jana katika uzinduzi wa Mpango Kazi wa Taifa wa
Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto wa miaka mitano 2017/18
hadi 2021/22 uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
kwenye uzinduzi huo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, Ummy Mwalimu alisema hatua hiyo inatokana na kuwepo vitendo
vya ubakaji pamoja na vitendo vya watoto wa kiume kulawitiana.
Aliongeza
kuwa licha ya kuwepo walimu wa nidhamu lakini wamekuwa wakiogopwa hivyo
madawati hayo yatakuwa ni rafiki pindi mtoto anapokutana na vitendo
hivyo anakimbilia katika dawati hilo.
Alifafanua
kuwa kamati za ulinzi na usalama wa mtoto kwa kila mtaa na kijiji
pamoja na kuanzisha mtandao wa wanaume katika kila kata ambao watakuwa
wakitetea na kulinda vitendo vya ukatili.
“Ukatili
mashuleni tunazungumzia ubakaji wa wakubwa, kinachosikitisha watoto wa
kiume wanalawitiana katika mazingira ya shule, sisi kama wizara tumeona
tuanzishe dawati la kuwalinda watoto katika shule zetu zote za msingi na
sekondari,” alisema.
Akizungumza
kwenye mkutano huo, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini,
Alvaro Rodriguez alisema dhamira ya serikali imechangia katika kuifanya
Tanzania kuwa nchi ya kwanza katika Bara la Afrika chini ya mpango mpya
wa ushirikiano wa kimataifa katika kukomesha ukatili dhidi ya watoto.
Rodriguez
alisema malengo ya dunia yanataka kumaliza vitendo vya ukatili kwa
wanawake na watoto na badala yake kuwekeza katika kuwawezesha na
kuwalinda.
Alisema UN itaendelea kushirikiana na serikali katika kuzuia ukatili wa aina yoyote kwa wanawake na watoto.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliagiza wizara, taasisi za
serikali, mikoa, wilaya pamoja na mamlaka za mitaa, kuhakikisha
zinazingatia mpango kazi huo kwa kutenga fedha katika bajeti zao kuanzia
mwaka wa fedha 2017/18 ili kukidhi utekelezaji wa mpango huo.
Alisema
utekelezaji wa mpango huo utagharimu Sh bilioni 267.4 kwa miaka mitano,
ambapo unatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo,
sekta binafsi na wananchi kwa ujumla.
Kwa
upande wake, waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi,
Ajira, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama alisema mpango huo ni muhimu
kwa taifa hasa kwa wakati huu, kwa kuwa vitendo vya unyanyasaji vimekuwa
vikiongezeka.
Alisema
imefika mahali ambapo vitendo hivyo vinatakiwa vikome na kwamba Ofisi
ya Waziri Mkuu itasimamia mpango kazi huo ili kuhakikisha unatekelezeka
na kuendana na gharama halisi ili kufikia malengo.
Waziri
wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe alisema serikali inataka
kupitia sheria ya mtoto ya mwaka 2009 ili kubaini mapungufu ambyo wadau
wameyaona na kuyafanyia marekebisho.
Alisema
pia wanaangalia namna ya kupanua wigo wa fursa kwa wanawake na watoto
katika kutafuta haki na hatua mojawapo ya kufanikisha suala hilo ni
kuanzisha mfumo wa msaada wa kisheria kwa wananchi wasio na uwezo.
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Stella Manyanya alisema
kuwa katika kutekeleza mpango huo, wizara hiyo itahakikisha inasimamia
ipasavyo katika maeoneo yote inayohusika.
Naye
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani alisema, lengo la
serikali ni kuhakikisha wanapeleka umeme katika vijiji vyote kupitia
REA awamu ya tatu hasa katika zahanati ili kuwasaidia akinamama
kujifungua katika mazingira salama.
Aidha,
pia alisema shule nyingi zinaungua kutokana na matumizi ya vibatari
hivyo wamekusudia kufikisha umeme katika shule zote. Dk Kalemani pia
aliwaonya wamiliki wa migodi ambao wamekuwa hawawashirikishi wanawake
katika shughuli za kiuchumi.
Naibu
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura
alisema wizara yake itatumia idara za sanaa na utamaduni ili kuhakikisha
wanatokomeza vitendo vya ukatili.
Kwa
upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
alimwakilisha waziri wa wizara hiyo, Mwigulu Nchemba alisema matukio ya
ukatili yamekuwa ni mengi, na kuahidi kuwa wizara itaendelea kuhakikisha
wanatumiwa wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Mawaziri
wengine waliozungumza katika mkutano huo ni Waziri wa Kilimo, Mifugo na
Uvuvi, Dk Charles Tizeba, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji,
Charles Mwijage. Wizara nyingine zinazoshiriki ni Ofisi ya Rais,
TAMISEMI.
Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii. Jinsia na Watoto Mh. Ummy Mwalimu
akizungumza na wadau (hawapo pichani) kwa niaba ya Makamu wa Rais, Mama
Samia Suluhu Hassan kabla ya uzinduzi wa Mpango Kazi wa Taifa wa
Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto jijini Dar es Salaam .
Waziri
wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mh. Jenista Joakim
Mhagama akiongea na wadau (hawapo pichani) kabla ya uzinduzi wa Mpango
Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto jijini
Dar es Salaam
Waziri
wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mh. Charles Mwijage akiongea na wadau
(hawapo pichani) kabla ya uzinduzi wa Mpango Kazi wa Taifa wa
Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto jijini Dar es Salaam
Waziri
wa Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe akiongea na wadau (hawapo
pichani) kabla ya uzinduzi wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili
Dhidi ya Wanawake na Watoto jijini Dar es Salaam
Mratibu
Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la
Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akiongea na wadau (hawapo
pichani) kabla ya uzinduzi wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili
Dhidi ya Wanawake na Watoto jijini Dar es Salaam
Naibu
Waziri Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mh. Anastazia Wambura
akiongea na wadau (hawapo pichani) kabla ya uzinduzi wa Mpango Kazi wa
Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto jijini Dar es
Salaam
Naibu
Waziri Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mh. Anastazia Wambura (Kulia)
akifurahia jambo na kwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
Injinia Stella Manyanya baada ya uzinduzi wa Mpango Kazi wa Taifa wa
Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto jijini Dar es Salaam .
(Picha zote na Benjamin Sawe-Maelezo)
Sign up here with your email
ConversionConversion EmoticonEmoticon