KIKAO
cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kinakutana leo jijini Dar es Salaam ikiwa ni kikao cha kwanza kuongozwa
na Rais John Magufuli tangu achaguliwe kukiongoza chama hicho tawala
Julai mwaka huu.
Juzi, Rais Magufuli aliongoza kikao cha Kamati Kuu ambacho kilipaswa kuwa cha siku mbili, lakini kikamaliza kazi zake juzi.
Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Nape Nnauye aliwaambia waandishi wa
habari juzi baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati Kuu kwamba
mapendekezo au hoja zote zilizoibuliwa na wajumbe katika kikao hicho
zitawasilishwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ambacho
kitafanyika jijini Dar es Salaam.
Nape
hakueleza hoja na mapendekezo hayo yanayopelekwa NEC, lakini kwa ujumla
kikao hicho ndicho chenye uamuzi wa kubariki mapendekezo yanayotoka
katika kikao cha Kamati Kuu hivyo inatarajiwa kuwa itafanya maamuzi
mbalimbali.
Miongoni
mwa hayo ni uteuzi wa mgombea wa ubunge wa Jimbo la Dimani Zanzibar,
lakini pia huenda NEC ikabariki uteuzi wa wajumbe wa Sekretarieti ya
chama hicho kama yatawasilishwa kwao na Mwenyekiti kutokana na nafasi
mbalimbali kuwa wazi.
Naibu
Katibu Mkuu Bara, Rajab Luhavi na aliyekuwa Kaimu Katibu wa NEC wa
Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Dk Pindi Chana hivi karibuni wameteuliwa
kuwa mabalozi wakati Nape pia anashikilia wadhifa wa uwaziri wa Habari,
Sanaa, Utamaduni na Michezo.
Aidha,
aliyekuwa Msemaji wa chama, Christopher ole Sendeka mwishoni mwa wiki
aliteuliwa na kuapishwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, hali inayoashiria
kuwa mabadiliko katika Sekretarieti hayaepukiki.
Aidha,
Nape aliwaambia waandishi juzi kuwa ajenda kuu katika kikao hicho cha
Kamati Kuu ilikuwa ni tathimini ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Alisema
tathimini hiyo ilikuwa ni pana na imefanyika kwa kipindi cha karibu
mwaka mmoja ambayo ilifanyika kwa ngazi ya mikoa, wilaya na kata na
wamemaliza tathimini na kuipeleka makao makuu ya chama ili kupitiwa na
vikao vya maandalizi vya sekretarieti na vikao vingine kisha
ikawasilishwa kamati kuu kwa ajili ya kujadiliwa.
Alisema
baada ya tathimini hiyo kujadiliwa Kamati Kuu itapelekwa katika kikao
cha Halmashauri Kuu leo ambacho ndio chenye maamuzi na kitapitia na
kuangalia endapo kuna mambo yaliyopendekezwa na hatua za kuchukua kama
mabadiliko na vitu vingine.
“Huu
ni utaratibu wa kawaida katika chama chetu kila uchaguzi huwa
inafanyika tathimini ambazo hutusaidia sana, kujua wapi tulifanya vizuri
na wapi hatukufanya vizuri na mengineyo yote yaliyokuwa sehemu ya
ushiriki wa chama katika Uchaguzi Mkuu, na tumekuwa tukifanya hivi
katika chaguzi zote hali ambayo imeifanya CCM kuimarika zaidi,” alieleza
Nape.
Sign up here with your email
ConversionConversion EmoticonEmoticon