Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema
Kenya ni nchi inayoongoza kwa uwekezaji nchini Tanzania ikilinganishwa
na nchi nyingine za Bara la Afrika.
Rais
Magufuli amesema hayo leo tarehe 31 Oktoba, 2016 katika mkutano na
waandishi wa habari uliofanyika katika Ikulu ya Nairobi nchini Kenya
ambako ameanza ziara ya Kiserikali ya siku mbili kwa mwaliko wa Rais wa
Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta.
Rais
Magufuli ambaye kabla ya Mkutano huo na waandishi wa habari amepokelewa
rasmi kwa kupigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa
kwa heshima yake na baadaye kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake
Rais Uhuru Kenyatta, amesema takwimu za kituo cha uwekezaji Tanzania
(TIC) zinaonesha kuwa Kenya ina jumla ya kampuni 529 zinazoendesha
shughuli zake nchini Tanzania ambapo zimewekeza Dola za Marekani Bilioni
1.7 na zimeajiri watu 56,260.
Pia,
Rais Magufuli amebainisha kuwa biashara kati ya Tanzania na Kenya
imeongezeka kutoka Shilingi za Kitanzania Bilioni 652.9 hadi Shilingi za
Kitanzania Trilioni 2.044.
“Naomba
niwahakikishie kuwa uhusiano na ushirikiano wetu ni mzuri na utaendelea
kuwa mzuri zaidi, na kwetu sisi Tanzania, Kenya ndio nchi ya kwanza kwa
uwekezaji kuliko nchi zote za Afrika.
“Tunashirikiana
vizuri katika uchumi, watu wetu wanafanya kazi pamoja, yapo makabila
yetu ambayo yanaingiliana kwa shughuli zao za kila siku na hata
wanyamapori wetu wanazunguka katika nchi zote mbili bila kujali mipaka” amesema Rais Magufuli.
Dkt.
Magufuli amesisitiza kuwa Serikali yake itaendeleza na kuimarisha zaidi
uhusiano na Kenya ulioasisiwa na Rais wa Kwanza wa Tanzania Hayati
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais wa Kwanza wa Kenya Hayati Mzee
Jomo Kenyatta na amewakaribisha wafanyabiashara wengi zaidi wa Kenya
kuwekeza nchini Tanzania.
“Kabla
ya kuja hapa nimekwenda kutoa heshima katika kaburi la Mzee Jomo
Kenyatta, kwa kweli nimeguswa sana na kazi kubwa iliyofanywa na wazee
wetu, naomba niwahakikishie kuwa tunawathamini sana ndugu zetu Wakenya
na tutaendelea kufanya hivyo” amesisitiza Dkt. Magufuli.
Kwa
upande wake Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta amemshukuru
Rais Magufuli kwa kukubali mwaliko wake na amemhakikishia kuwa Kenya
itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano na Tanzania.
“Kwetu
sisi Tanzania ni ndugu zetu, ni kaka na dada zetu tunao ushirikiano wa
siku nyingi na wa kidugu na tutahakikisha tunauendeleza ushirikiano na
uhusiano huu mzuri ulioasisiwa na wazee wetu” amesema Mhe. Kenyatta.
Rais
Kenyatta amesema Tanzania na Kenya ni nchi zinazofanana kwa mambo mengi
muhimu ikiwemo kubadilishana uongozi wa Serikali kwa njia ya amani na
ameongeza kuwa katika mazungumzo yao wamekubaliana kuwa nchi hizi
zitaendelea kuzisaidia nchi nyingine za Afrika Mashariki zinazokabiliwa
na matatizo mbalimbali.
Aidha,
Rais Kenyatta amesema Kenya itaendelea kushirikiana na Tanzania katika
kutekeleza miradi ya ushirikiano ikiwemo ujenzi wa miundombinu kama vile
barabara ya Bagamoyo (Tanzania) hadi Malindi (Kenya) pamoja na mambo
mengine ambayo Tume ya pamoja ya ushirikiano kati ya nchi hizi mbili
(Joint Commission Cooperation) itayaainisha.
Baadaye
leo, Rais Magufuli anatarajiwa kuhudhuria dhifa ya kitaifa katika Ikulu
ya Nairobi aliyoandaliwa na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta na Kesho
anatarajiwa kutembelea kiwanda cha maziwa cha Eldoville kilichopo Karen
Jijini Nairobi, na kuzindua barabara mchepuko ya Southern By-pass
iliyopo Jijini Nairobi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Nairobi
Sign up here with your email
ConversionConversion EmoticonEmoticon