Waziri
 Mkuu Kassim Majaliwa jana aliongoza mamia ya waombolezaji kuaga mwili 
wa marehemu Mzee Xavery Pinda ambaye ni baba mzazi wa Waziri Mkuu 
Mstaafu Mheshimiwa Mizengo Pinda.
Akizungumza wakati wa kuaga mwili huo nyumbani kwa Mheshimiwa Pinda kijijini Zuzu, Manispaa ya Dodoma jana Waziri Mkuu alitoa pole kwa wanafamilia na kuwaomba waendelee kumuombea marehemu apumzike mahala pema peponi.
Mzee
 Xavery alifariki dunia Novemba 27, 2016 saa 9.30 alasiri katika 
Hospitali ya Mkoa wa Dodoma alikokuwa amelazwa akipatiwa matibabu.
Alisema
 msiba huo ni mzito, hivyo anawaomba wanafamilia wawe watulivu na moyo 
wa subira katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao.
Wakati
 huo huo Waziri Mkuu alimuhakikishia Mheshimiwa Pinda kwamba Serikali 
iko pamoja naye katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mzazi wake.
Naye
 Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dk. Jakaya Kikwete alisema marehemu Mzee 
Xavery alikuwa mwema sana na alikuwa na upendo kwa watu wote.
“Baba yake Pinda alikuwa baba yangu pia. Alitambua ugumu wa kazi tulizokuwa tunazifanya na alitutaka tuwe wavumilivu,” alisema.
Kwa
 upande wake Mheshimiwa Pinda aliwashukuru viongozi wa Serikali, vyama 
vya siasa na wananchi kwa kutenga muda wao na kwenda kumfariji kufuatia 
msiba huo mzito. “Kuondokewa na baba mzazi au mwanafamilia yeyote si 
jambo dogo”.
Awali
 akisoma wasifu wa marehemu, Edward Kyungu ambaye ni mjukuu alisema Mzee
 Xavery alizaliwa mwaka 1926 katika kitongoji cha Mbede akiwa ni mtoto 
wa pekee wa Mzee Mizengo Pinda na Mama yake Wakalyate (Umartina).
Mzee Xavery alikuwa Katekista kazi ambayo aliifanya kuanzia mwaka 1951 hadi 1972 alipoamua kustaafu.
“Kazi
 ya pili ambayo alianza kuifanya kabla na hata wakati wa Ukatekista ni 
ukulima, jambo ambalo amewarithisha  watoto wake wote na ndio maana 
wameachiwa sifa moja ya kuitwa watoto wa mkulima,” alisema.
Mzee
 Xavery anatarajiwa kuzikwa leo Alhamisi, Desemba Mosi, 2016 katika 
kijiji cha Kibaoni wilaya ya Mlele mkoani Katavi. Marehemu ameacha mke, 
watoto wanane, wajukuu 54 na vitukuu 40.
Sign up here with your email





ConversionConversion EmoticonEmoticon